Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG. 
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekabidhi mradi wa uunganishaji wa gesi asilia kutoka katika bomba kubwa la gesi asilia linalomilikiwa na TPDC kwenda kwenye bomba dogo la usambazaji wa gesi asilia kutoka Ubungo hadi Mikocheni ambalo nalo linamilikiwa na TPDC ili kuongeza kiasi cha gesi asilia katika bomba hilo kwa lengo la kuwafikia watumiaji wengi zaidi. 

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba akikabidhi jukumu la ujenzi wa mradi wa uunganishwaji wa gesi asilia kutoka kwenye bomba kubwa la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam katika eneo la Valvu namba 15 (Block Valve Station-BVS) ambapo ndipo bomba hilo litarajiwa kujengwa hadi eneo la Ubungo Maziwa litakapounganishwa na bomba dogo la usambazaji wa gesi asilia kuelekea Mikocheni Dar es Salaam. 

“Leo ni siku kubwa sana kwetu kama Kampuni ya Mafuta ya Taifa tunapokabidhi rasmi jukumu la ujenzi wa miundombinu ya kutoa gesi asilia kutoka kwenye bomba letu kubwa kwenda kwenye bomba letu dogo la usambazaji wa gesi asilia kazi ambayo itafanywa na kampuni ya SINOMA ambayo faida yake kubwa ni kulipa uwezo wa kubeba na kusambaza gesi nyingi zaidi itakayoruhusu uunganishwaji zaidi wa gesi asilia kwa watumiaji wapya katika maeneo yote ambayo bomba hilo linapita yaani Ubungo, Sinza, Chuo Kikuu, Survey, Mwenge na Mikocheni” alifafanua Kaimu Mkurugenzi. 

Akizungumzia wanufaika wa mradi huo pindi utakapokamilika, ndugu Musomba amesema kuwa, pamoja na kuendelea kusambaza kwa watumiaji wa zamani ambao ni MM I, MM II, MM III, TanPack na Iron and Steel wateja wapya watakaonufaika ambao tayari wameshakubaliana ni Coca Cola kwanza Limited na BIDCO na nyumba 70 katika awamu ya kwanza na kwamba wanatarajia kuunganisha kwa viwanda zaidi vitakavyokuwa tayari kwa muda wowote. 

Aidha akieleza kuhusu utaratibu wa uunganishwaji wa gesi asilia kwa watumiaji Mhandisi Musomba ameeleza kuwa, “Utaratibu ni wa kawaida sana kikubwa mteja tarajiwa anatakiwa kuwasilisha barua ya maombi ya gesi asilia kisha wataalam kufanya utafiti wa namna ya kumuunganishia mteja gesi hiyo na kwa upande wa watumiaji wa majumbani tunashauri pia nyumba kadhaa kuungana pamoja na kuleta barua kisha taratibu za kiutalamu za namna ya kuwafikishia gesi asilia zifanyike.” 

Kwa upande wake Meneja Mkuu Msaidizi wa SINOMA, Lu Xiaoqiang ambao ndio Wakandarasi walioshinda zabuni ya ujenzi wa mradi huo amesema kuwa, “Leo ni siku ya furaha kwa kuwa tumeweza kupata nafasi ya kutekeleza mradi wa TPDC wa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka eneo la Ubungo bomba ambalo tunaamini litasaidia kukuza uchumi wa nchi nzuri ya Tanzania kwa kusambaza nishati viwandani na majumbani.” 
Akizungumzia gharama za matumizi ya gesi asilia majumbani Mhandisi Musomba amefafanua kuwa, “Matumizi ya gesi asilia ni ya gharama nafuu kulinganisha na mkaa na gesi za mitungi-LPG ambapo kwa mtumiaji wa gesi za mitungi mfano wa Kilo 15 ambayo itatumika kwa mwezi mmoja kama akitumia gesi asilia atatumia hadi miezi miwili na hivyo kuokoa karibu nusu ya gharama ya matumizi ya nishati majumbani lakini pia gesi asilia ni nyepesi kuliko hewa na hivyo kuwa salama zaidi kwa matumizi hata pale inapovuja kwa kuwa hupotea hewani.

” Jukumu la kusambaza gesi asilia ni la msingi kwa maeneo ya uchumi imara wa viwanda na hivyo TPDC inaendelea kufanya tafiti za kitaalamu za usambazaji wa gesi asilia katika maeneo mengine ya nchi yakiwemo Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga na Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba akieleza kwa kina Mradi Mpya wa Kuunganisha gesi asilia kutoka bomba kubwa hadi kwenye bomba dogo la Ubungo Mikocheni mradi ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi miwili. Piv
Meneja Mkuu Msaidizi wa SINOMA, Lu Xiaoqiang akielza kwa waandishi wa habari namna watakaovyotekeleza ujenzi wa Miundombinu hiyo kwa ufanisi na wakati kadiri ya masharti ya mkataba. Pembeni yake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Ubungo Tanesco, Sophia Fitina akielezea jinsi walivyoupokea mradi huo tokea umeingia katika eneo lao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba (wa tatu toka kushoto) akiwa na  Meneja Mkuu Msaidizi wa SINOMA ndugu Lu Xiaoqiang (anayemfuatia Kushoto) pamoja na wafanyakazi wanaotekeleza mradi huo. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...