Na. Jeshi la Polisi.

Kampuni binafsi za ulinzi zinazoendesha shughuli zake hapa nchini zimetakiwa kuvaa sare za aina moja ifikapo Januari Mosi mwakani kwa lengo la kuondoa sare ambazo zimekuwa zikifanana na zinazovaliwa na askari wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Kamisheni ya Ushirikishwaji wa Jamii, Mussa Alli Mussa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa kikao kilichowakutanisha wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi.

Kamishna Mussa amesema sare zilizokubaliwa kwa pamoja kati ya Jeshi la Polisi na wawakilishi wa kampuni binafsi za ulinzi zinatakiwa ziwe na rangi ya bluu nyeusi (Dark blue), nyeusi pamoja na mashati meupe kulingana na mazingira ya kampuni inapofanyia ulinzi.

“Kampuni zote binafsi za ulinzi hakikisheni mnajiandaa mapema kwa kuwa muda utakapofika hakuna kampuni binafsi ya ulinzi itakayoruhusiwa kufanya kazi bila ya kutumia sare hizi ambazo zitakuwa ni utambulisho rasmi wa sekta hii binafsi ya ulinzi” Alisema Mussa.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi (TAPSCOA)  Bw. Shawiniaufoo Kimuto amesema kuwepo kwa aina moja ya sare kutasaidia kuondoa mgongano uliopo hivi sasa ambapo baadhi ya kampuni zinavaa sare zinazofanana na zinazovaliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kimuto alisema jambo hilo litasaidia kufahamika kwa urahisi kwa walinzi wa kampuni binafsi na hivyo kuwa rahisi kupata msaada pindi wanapotekeleza majukumu yao ya kulisaidia Jeshi la Polisi kuhakikisha usalama unakuwepo katika maeneo wanayofanyia kazi.

Naye Julieth Rushuli kutoka kampuni binafsi ya ulinzi ya 4JY amesema Sekta binafsi ya ulinzi imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa usalama unaimarika katika maeneo yao hivyo jamii inapaswa kuwapa ushirikiano pindi wanapotekeleza majukumu yao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...